Menu
RSS
Africa

Maaskofu wavipongeza vyama vya siasa kwa uungawana

 

JOHANNESBURG, Afrika Kusini

 

BARAZA la Maaskofu Katoliki Afrika Kusini (SACBC) limevipongeza vyama vya siasa nchini humo kwa jinsi vilivyopokea na kukubali matokeo ya uchaguzi uliofanyika hivi karibuni.

 

Pongezi hizo zimo kwenye Waraka wa Kichungaji uliotolewa na SACBC kufuatia utulivu uliooneshwa na vyama vyote vya siasa nchini humo baada ya kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

 

Katika waraka huo, Maaskofu walisema, wamefurahishwa kwa namna vyama vya siasa vilivyopokea na kuyakubali matokeo ya uchaguzi huo kisha uliofanyika uliofanyika Agosti 3, 2016 na kuridhia kuwa ulikuwa huru na wa haki.

 

Walisema, kitendo kilichooneshwa na vyama vya siasa katika uchaguzi huo kinadhihirisha kukomaa kwa demokrasia na kwamba huo ushindi kwa demokrasia yenyewe.

 

“Kitendo kilichooneshwa na vyama vya siasa katika uchaguzi huu kinadhihirisha kukomaa kwa demokrasia na kwa kweli huu ni ushindi kwa demokrasia yenyewe” walibainisha Maaskofu katika waraka wao huo.

 

Walisema, uchaguzi huo unatakiwa kutamalaki katika awamu mpya ya historia ya demokrasia nchini Afrika Kusini ukihusisha Serikali ya Mseto, upinzani wa kweli wa kisiasa na uwajibikaji mkubwa katika matumizi ya madaraka.

 

Waraka huo ulieleza kuwa uchaguzi huo umeonesha kupungua kuungwa mkono kwa chama tawala cha African National Congress (ANC), kilichokuwa kikihodhi siasa za nchi hiyo, na hiyo ni dalili kuwa wananchi wana hamu ya kuona mabadiliko yakitokea.

 

Maaskofu walisema, katika uchaguzi huo, wananchi wamezungumza kwa kura, wameonesha kuwa wanahitaji mabadiliko, wanataka huduma na wamechoka na rushwa, ufisadi, matumizi mabaya ya madaraka na hawataki kupuuzwa.

 

“Katika uchaguzi huo, wananchi wamezungumza kwa kura, wameonesha kuwa wanahitaji mabadiliko, wanataka huduma na wamechoka na rushwa, ufisadi, matumizi mabaya ya madaraka na hawataki kupuuzwa” walibainisha Maaskofu.

 

Katika uchaguzi huo, vyama vya upinzanai vya Democratic Alliance (DA) na the Economic Freedom Fighters, vilionesha upinzani mkubwa kwa ANC kiasi cha kupoteza umeya katika Jiji la Johannesburg.

 

Pakistan yateua Waziri Mkatoliki kuimarisha uhusiano

 

 

 

KARACHI, Pakistan

 

MJUMBE wa Baraza la Mawaziri wa Jimbo la Sindh nchini Pakistan, Anthony Naveed, amepandishwa hadhi kuwa Msaidizi Maalum wa Waziri Mkuu akipewa jukumu mahsusi la kusimamia ofisi ya maelewano kati ya dini mbalimbali. 

 

Naveed anakuwa mjumbe wa kwanza Mkatoliki kutoka Sindh kufikia wadhifa huo na anakuwa Mkatoliki pekee kwenye Baraza la Mawaziri la Waziri Mkuu Syed Murad Ali Shah.

 

Akizungumzia uteuzi huo, Naveed, anayetoka Chama cha Watu wa Pakistan (Pakistan People’s Party), alisema, atatumia nafasi aliyopewa kuimarisha maelewano kati ya watu wa Dini mbalimbali katika nchi hiyo inayokabiliwa na misimamo mikali ya imani.

 

Alisema, tangu mwaka 2012, Serikali katika Jimbo la Sindh imekuwa ikijitahidi kupigania maelewano kati ya Dini mbalimbali na kujenga jamii yenye kuvumiliana kwa watu wenye tofauti ya Dini, imani na madhehebu.

 

“Tangu mwaka 2012, Serikali yao katika Jimbo la Sindh imekuwa ikijitahidi kupigania maelewano kati ya Dini mbalimbali na kujenga jamii yenye kuvumiliana kwa watu wanaotofautiana kwa Dini, imani na madhehebu” alisema Naveed.

 

Alisema, ilikuwa kazi ngumu na haikuwa rahisi wala mchezo kuwakusanya na kuwaweka pamoja watu wa Dini na imani tofauti lakini jambo hilo limefanyika kwa mafanikio katika Jimbo la Sindh.

 

Naveed alisema, hatua inayofuata sasa ni kuandaa warsha na semina kwa ajili ya viongozi wa Dini wa madhehebu mbalimbali na kuunda vikundi katika ngazi ya wilaya ili kuwezesha kuwepo kwa maelewano ya kidini katika ngazi ya chini.

 

“Hatua inayofuata sasa ni kuandaa warsha na semina kwa ajili ya viongozi wa Dini wa madhehebu mbalimbali na kuunda vikundi katika ngazi ya wilaya ili kuwezesha kuwepo kwa maelewano ya kidini katika ngazi ya chini” alibainisha Naveed.

 

Naveed amekuwa mtetezi wa haki za binadamu wa aina ya pekee mwenye rekodi ya pekee katika jitihada za kulinda na kutetea haki za Wakristo nchini Pakistan.

 

Akiwa mwanasiasa, Naveed aliyekuwa pia mwanachama mkereketwa wa Tume ya Vijana Wakatoliki katika Jimbo Kuu Katoliki la Karachi kati ya mwaka 1998 na 2005, amejitesa kuhakikisha Wakristo walio wachache wanapata haki za msingi za kikatiba katika nchi hiyo yenye Waislamu wengi.

 

Kanisa lanusurika kulipuliwa

 

 

 

JAKARTA, Indonesia

 

JENGO la Kanisa Katoliki la Parokia moja nchini Pakistan limenusurika kulipuliwa baada ya milipuko aliyokuwa nayo mlipuaji wa kujitoa mhanga kushindwa kulipuka.

 

Msemaji wa Polisi nchi humo, Meja Jenerali Boy Rafli Amar alisema kuwa mlipuaji huo wa kujitoa mhanga aliingia na milipuko hiyo kanisani wakati kukiwa na umati mkubwa wa waamini walikokusanyika kwa ajili ya ibada ya Misa ya Dominika.

 

Meja Jenerali Amar alisema, mtu huyo kabla ya kutaka kufanya tukio hilo, Jumapili Agosti 28, 2016, alidhibitiwa ingawa alifanikiwa kumjeruhi Padri aliyekuwa akiadhimisha Misa Takatifu.

 

Alisema, tukio hilo lilifanyika wakati ibada ya Misa Takatifu ikiendelea katika Kanisa la Mtakatifu Yosefu lililopo Medan, Mji Mkuu wa Jimbo la Kiserikali la Sumatra Kaskazini.

 

Meja Jenerali Amar alisema, wakati wa ibada hiyo, kijana mwenye umri wa miaka 17 anayejulikana kwa jina la Ivan Armadi Hasugian alisimama kwenye benchi alipokaa na kukimbilia altareni alikokuwa Padri.

 

Hata hivyo, Meja Jenerali Amar alisema, mabomu aliyokuwa nayo kijana huyo kwenye begi la mgongoni alilobeba yaliungua bila kulipuka kama ilivyokusudiwa.

 

“Hata hivyo, mabomu aliyokuwa nayo kijana huyo kwenye begi la mgongoni alilobeba yaliungua bila kulipuka kama ilivyokusudiwa” alisema Meja Jenerali Amar.

 

Alisema, kabla ya kudhibitiwa na waamini, kijana huyo alichomoa shoka alilokuwa nalo kwenye begi lake hilo na kumjeruhi mkononi, Padri Mwadhimishi Misa Albert Pandiangan mwenye umri wa miaka 60. 

 

Akizungumza na waandishi wa habari, Waziri wa Usalama, Wiranto, aalisema, upekuzi uliofanywa katika simu aliyokutwa nayo kijana huyo, limo jina la Abu Bakr al-Baghdadi, kiongozi wa Kundi la Islamic State (IS), la Mashariki ya Kati.

 

Wiranto alisema, kijana huyo aliwaambia polisi waliokuwa wakimhoji kwamba yeye hayupo peke yake bali anafanyakazi na watu wengine ingawa hakutoa maelezo zaidi.

 

Masista wa Mama Teresa au Wamisionari wa Upendo

 

 

 

CALCUTTA, India

 

WAKATI Mwenyeheri Mama Teresa wa Calcutta akitangazwa kuwa Mtakatifu Jumapili Septemba 4, 2016, Dominika ya 23 ya Mwaka C wa Kanisa, Masista wa shirika alilolianzisha la Wamisionari wa Upendo {Missionaries of Charity}, wamemshukuru kwa kuanzisha shirika hilo.

 

Pongezi hizo zilitolewa na Mama Mkuu wa Shirika aliyechukua nafasi ya Mama Teresa, Sista Prema Pierick, alipokuwa akizungumzia namna Masista wa shirika hilo wanavyojivunia kazi iliyofanywa na mwanzilishi wao.

 

Sista Prema aliyekutana na Mama Teresa kwa mara ya kwanza miaka 36 iliyopita mnamo mwaka 1980, alisema, Mama Teresa ni kielelezo muhimu cha utendaji kazi katika shirika lao na Kanisa.

 

Alisema, Mama Teresa katika utume wake na katika maisha yake yote alijitoa kwa moyo wake wote kuwasaidia maskini kati ya maskini waliokithiri kwa umaskini.

 

Sista Prema alisema, utakatifu wa Mama Teresa umemfanya yeye na watawa wengine wa sshirika lao kujiona kuwa wakati wote mama huyo yupo pamoja nao katika utume wao.

 

Alisema, waliishi na Mama Teresa na kuichukulia hali hiyo kama ya kawaida na kujiona kwamba wakati wote mama huyo yupo pamoja na watawa na kuwasikiliza kwa makini.

 

“Tuliishi na Mama Teresa na tunaichukulia hali hii kama ya kawaida na kujiona kwamba wakati wote mama huyu yupo pamoja nasi na kutusikiliza kwa makini” alibainisha Sista Prema.

 

Alisema, wakati wa uhai wake, walifurahia uwepo wake na walitaka kufahamu kutoka kwake namna siku yake ilivyokuwa kila siku na namna alivyofanya kazi zake.

 

“Wakati wa uhai wake, tulifurahia uwepo wake na tulitaka kufahamu kutoka kwake namna siku yake ilivyokuwa kila siku na namna alivyofanya kazi zake” alisema Sista Prema.

 

Mama Teresa wa Calcutta alitangazwa kuwa Mwenyeheri, miaka sita baada ya kufariki dunia akiwa na umri wa miaka 87 na aliyekuwa Baba Mtakatifu wakati ule, Mtakatifu Yohana Paulo II, Oktoba 19, 2003.

 

Read more...

Kataeni ushawishi wa kukiuka maadili-Kanisa

 

ABUJA, Nigeria

 

WAKRISTO katika Bara la Afrika na watu wote wenye mapenzi mema wametakiwa kukataa kuyumbishwa katika misingi ya maadili na utu wema kama inavyobainishwa katika Maandiko Matakatifu.

Katika waraka wake wa kichungaji uliotolewa hivi karibuni, Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria lilidai kuwa kwa hali ilivyo sasa, Wakristo hawana budi kukataa kuyumbishwa katika imani.

Maaskofu walisema, mwelekeo unaoendelea kuoneshwa na mataifa ya Ulaya na Marekani wa kushabikia hatimaye kupitisha sheria zinazokiuka misingi ya maadili na utu wema, unatisha na kuhatarisha Kanisa Barani Afrika.   

Walitaja baadhi ya sheria zinazokiuka maadili kuwa ni kuruhusiwa kwa ndoa za jinsia moja kama ilivyofanyika hivi karibuni huko Ireland na nchini Marekani ambako Mahakama Kuu ilipitisha uamuzi wa kuruhusu ndoa za jinsia moja kwa nchi nzima.  

Katika waraka wao, maaskofu walisema, hayo yanayotokea ni dalili ya kukengeuka na kutopea katika dhambi kwa kisingizio kuwa ni uhuru wa mtu binafsi.

Walisema, waamini hasa vijana, hawana budi kujitenga na kila aina ya ushawishi wa kukataa misingi ya maadili na utu wema hatimaye kujitumbukiza katika sheria zinazopingana na misingi hiyo.

Maaskofu walisema, jambo hilo ni muhimu kwa kuwa wapo baadhi ya wanasiasa katika Bara la Ulaya wanaoshinikiza nchi zisizokuwa na sheria zinazokiuka maadili kuzipitisha.

 

Hadi sasa, ndoa za watu wa jinsia moja limekuwa jambo la kawaida nchini Marekani na katika baadhi ya nchi za Ulaya zikiwemo Ireland, Canada, Hispania na Ufaransa.  

Read more...

Serikali yakana kuwaua waandamanaji DRC

Serikali ya jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imekanusha madai ya kuwauwa waandamanaji waliokuwa wakiandamana kupinga mapendekezo ya kubadilisha sheria za uchaguzi mkuu.

Makundi ya kutetea haki za binadamu, yanasema kuwa zaidi ya watu arubaini wameuawa katika siku tatu za ghasia.

Waziri wa mawasiliano Lambert Mende, aliambia BBC kwamba polisi hawakutumia silaha zozote dhidi ya waandamanaji hao.

Alisema waandamanaji ambao aoliwataja kama waporaji, waliuawa na walinzi waliokuwa wanalinda majengo ya biashara yaliyoporwa

Mashirika ya kutetea haki za binadamu yanasema kwamba zaidi ya watu 40 wameuawa katika siku tatu za vurugu mjini Kinshasa.

Mabadiliko yaliyopendekezwa huenda yakachelewesha uchaguzi unaotarajiwa kufanyika mwaka ujao, wakati Kabila anatarajiwa kung'atuka baada ya kuitawala nchini huo kwa miaka 14.

Read more...

Watoto wa Hosni Mubarak kuachiliwa

Mahakama nchini Misri imeamrisha kuachiliwa kwa watoto wa kiume wa rais wa zamani Hosni mubarak wakati wanaposubiri kesi yao pamoja na baba yao inayohusu ufisadi.

Wakili wa Alaa na Gamal Mubarak anasema kwa anatarajia wawili hao kuachiliwa leo.

Hasira kutokana na kile kilichoonekana kama jitihada za kumuandaa Gamal Mubarak kuweza kumrithi babake kama rais ni moja ya sababu zilizosababisha maandamano makubwa yaliyomundoa madarakani rais Hosni Mubarak.

Read more...

Mahasimu wa Sudan Kusini wasaini makubaliano

Viongozi wa pande hasimu nchini Sudan Kusini wamesaini makubaliano ya kuimairisha juhudi za kukomesha vita vya wenyewe kwa wenyewe mjini Arusha, Tanzania, wakishuhudiwa na viongozi kadhaa wa Afrika.

Rais Salva Kiir na kiongozi wa waasi, Riek Machar, walisaini makubaliano hayo ambayo sasa yanazileta pamoja kambi mbili zinazopingana ndani ya chama tawala cha Vuguvugu la Ukombozi wa Sudan Kusini (SPLM).

Akizungumza baada ya kusainiwa kwa makubaliano hayo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania, Benard Membe, aliupongeza "uongozi wa SPLM kwa kufikia makubaliano ya kukiunganisha tena chama chao kwa maslahi ya Sudan Kusini."

Mazungumzo hayo yalikuwa chini ya usimamizi wa Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania, huku viongozi kadhaa wa mataifa jirani wakihudhuria kuhakikisha kuwa mahasimu hao wawili wanasaini makubaliano hayo.

Hadi sasa, hakuna taarifa za vipengele vya makubaliano hayo zilizotolewa, lakini makundi hasimu yanayowania udhibiti wa siasa za nchi hiyo yenye utajiri wa mafuta yameyavunja makubaliano ya kusitisha mapigano mara tano ndani ya kipindi cha mwaka mmoja uliopita.

IGAD yaendeleza juhudi za mapatano

 Mkutano wa upatanishi chini ya IGAD mwezi Novemba 2014 mjini Addis Ababa, Ethiopia.

Mkutano wa upatanishi chini ya IGAD mwezi Novemba 2014 mjini Addis Ababa, Ethiopia.

Mazungumzo hayo nchini Tanzania yalikuwa sehemu ya juhudi za pamoja kusaka makubaliano zilizoanzishwa na Jumuiya ya Ushirikiano wa Maendeleo ya Nchi za Mashariki na Pembe ya Afrika (IGAD) kwenye mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa.

Mazungumzo mengine ya IGAD yanatazamiwa kufanyika kandoni mwa mkutano wa kilele wa viongozi wa mataifa wanachama wa Umoja wa Afrika mjini Addis Ababa mwishoni mwa mwezi Januari.

Kwa mara ya kwanza, mapigano yalizuka kwenye taifa hilo jipya kabisa barani Afrika mwezi Disemba 2013, baada ya Kiir kumtuhumu makamu wake wa zamani, Machar, kutaka kumpindua. Baadaye yakageuka kuwa vita vya kikabila ndani ya SPLM na kuchochea mapigano ya kulipizana kisasi na mauaji nchi nzima yaliyopelekea vifo vya maelfu ya watu na kuirejesha nchi hiyo kwenye ukingo wa njaa na vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Kiir na Machar walikutana kwa mara ya mwisho mwezi Novemba mjini humo, ambako walikubaliana kusitisha mara moja vita, lakini makubaliano hayo yalivunjwa masaa machache tu baadaye.

Mapigano makali yaliripotiwa mapema wikik hii kati ya jeshi la waasi kwenye jimbo la kati la Lakes na siku ya Jumanne, msemaji wa jeshi, Philip Aguer, alivilaumu vikosi vya Machar kwa kukiripua kinu cha kuzalishia mafuta kwenye jimbo la Unity.

Hakuna orodha rasmi ya vita iliyorikodiwa na serikali au waasi au Umoja wa Mataifa, lakini taasisi ya kushughulikia mizozo duniani, International Crisis Group, inakisia kuwa kiasi cha watu 50,000 wameshapoteza maisha hadi sasa.

Read more...

Jitihada za Zimbabwe katika kuzindua sarafu yake ya dola

Mwaka 2009, Zimbabwe ililaazimika kuachana na dola yake ambayo hakuna alietaka kuitumia, na kuanza kutumia dola ya Marekani ili kuepusha kuanguka kwa uchumi wake na mfumuko wa bei wa kiwango cha juu kabisa.

Na sasa hakuna anaetaka kutumia sarafu zilizoingizwa kwenye mzunguko mwezi uliyopita.

Maamuzi ya kuitumia dola ya Kimarekani, kama sarafu rasmi ya nchi kama ilivyofanya Ecuador yanazusha maswali kuhusu ugavi wa fedha, sera ya fedha na hata uhuru wa taifa.

Kitendawili cha sarafu ya Zimbabwe kinabainisha pia ugumu wa kila siku wanaokabiliana nao wakati uchumi wao unapoelekea kwenye njia kama hiyo.

Noti za Marekani zinapatikana kirahisi, lakini kupata sarafu za dola ya Marekani na kuziweka katika mzunguko ni jambo tofauti

Kwa hiyo Gavana wa Benki kuu ya Zimbabwe John Mangudya alianzisha sarafu zilizopewa jina na 'bond coins' mwezi uliopita. Jina hilo limetokana na dhamana za dola milioni hamsini, zilizotolewa kwa ajili ya kuzichapisha na kuzisafirisha kutoka nchi jirani ya Afrika Kusini

Read more...

Shell kuwafidia Wanigeria dola milioni 84

Kampuni ya Shell italipa fidia ya dola milioni 84 kufuatia kuvuja kwa mabomba ya mafuta nchini Nigeria, hatua inayoweza kufungua njia ya kufidiwa hasara zinazosababishwa na kampuni za mafuta duniani.

Wanavijiji 15,600 kwenye jimbo la Niger Delta watapata dola 3,300 kila mmoja, huku dola milioni 30 zikiingizwa kwenye mfuko wa jamii kwa ajili ya maendeleo ya vijiji vyao.

Hata hivyo, kampuni ya uwakili ya Leigh Day jijini London, Uingereza, ambayo ndiyo iliyofikia makubaliano hayo na Shell kwa niaba ya wakulima hao wa Nigeria, ilisema ni jambo linalokera kwamba imechukuwa miezi sita kwa kampuni tanzu ya SPDC kukubali kwamba ilifanya makosa na kufikia makubaliano ya fidia.

Pamoja na kukiri kwamba makosa kwenye ufungaji wa mabomba ulisababisha kuvuja kwa mafuta, Shell imeendelea kusisitiza kwamba sehemu kubwa ya uharibifu wa mazingira nchini Nigeria husababishwa na hujuma dhidi ya mabomba hayo, uchimbaji haramu wa mafuta na majaribio ya wizi.

Read more...

GaUchaguzi wa Nigeria wachochea mashambulizi

Wizara ya mambo ya nje ya Marekani imesema uchaguzi mkuu ujao nchini Nigeria ni suala linalochangia kuongezeka pakubwa mashambulizi yanayofanywa na kundi la Boko Haram kaskazini mwa Nigeria.

 

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani Marie Harf amesema chaguzi za rais na ubunge nchini Nigeria zinazotarajiwa kufanyika tarehe 14 mwezi ujao zinapaswa kuendelea licha ya ghasia zilizoikumba nchi hiyo ambazo Umoja wa Mataifa na mashirika ya kutetea haki za binadamu yamesema zimewalazimu takriban watu 20,000 kutorokea nchi jirani katika siku chache zilizopita.

Harf amesema Marekani inaamini kuwa uchaguzi huo wa Februari umechangia katika kuongezeka katika visa vya mashambulizi kutoka kwa waasi wa Boko Haram.

Mashambulizi ya Boko Haram yaongeza taharuki

Uchaguzi huo unatarajiwa kuwa kinyang'anyiro kati ya Rais Goodluck Jonathan na mpinzani wake mkuu Muhammadu Buhari. Boko Haram inaaminika kutumia kipindi hiki cha uchaguzi kuchochea hali ya taharuki miongoni mwa raia kama mojawapo ya mikakati yake ya kutanua uasi.

 Wagombea urais Nigeria Muhammadu Buhari na Rais wa sasa Goodluck Jonathan

Wagombea urais Nigeria Muhammadu Buhari na Rais wa sasa Goodluck Jonathan

Tume ya uchaguzi nchini Nigeria hapo jana ilisema itaandaa uchaguzi katika majimbo matatu ya kaskazini mwa nchi hiyo ambayo ni ngome ya Boko Haram lakini imeonya kuna matumaini finyu kuwa watu watajitokeza kupiga kura katika eneo hilo.

Waasi wa Boko Haram waliuvamia mji wa Baga mnano tarehe tatu mwezi huu na kuwauwa maelfu ya wakaazi wa mji huo. Wafanyakazi wa mashirika ya kutoa misaada wameshindwa kuingia mji huo kuthibitisha idadi kamili ya waliouawa huku maiti zikizidi kuoza katika barabara za mji huo.

Umoja wa Afrika umelaani vikali mashambulizi hayo mabaya zaidi kuwahi kufanywa na Boko Haram tangu ianzishe uasi kaskazini mwa Nigeria mwaka 2009.

Rais wa Halmashauri ya Umoja wa Afrika Nkosazana Dlamini Zuma amesema ameshtushwa na mauaji ya Baga na miripuko ya mabomu yaliyotokea Potsikum pamoja na kuhusishwa kwa washambuliaji wa kike wa kujitoa muhanga na mtoto wa miaka kumi na kuzitaka nchi za Afrika na jumuiya ya kimataifa kuja pamoja na kukabiliana na kitisho cha Boko Haram.

Wanigeria wakimbilia Chad

Msemaji wa shirika la kushughulikia maslahi ya wakimbizi la umoja wa Mataifa UNHCR William Spindler amewaambia wanahabari kuwa asilimia sitini ya wanigeria wanaotorokea Chad ni wanawake na wasichana na kuongeza watoto 84 ambao hawakuandamana na watu wazima pia wameingia nchini humo.

 Mwanajeshi akishika doria katika mji wa Baga katika jimbo la Borno

Mwanajeshi akishika doria katika mji wa Baga katika jimbo la Borno

Msemaji wa shirika la umoja wa Mataifa la kutetea haki za binadamu Ravina Shamdasani amewaambia wanahabari mjini Geneva kuwa licha ya kutokuwepo kwa taarifa kamili kuhusu shambulizi la Baga,ni bayana kuwa kulifanyika mauaji ya watu wengi na kwamba wakaazi wengi wa mji huo wamelazimika kuyahama makaazi yao.

Shamdasani amesema kushambuliwa kimakusudi kwa raia kunakiuka sheria za kimataifa na wanatiwa wasiwasi na ripoti kuwa watoto na wazee ni miongoni mwa waathiriwa wa mashambulizi ya Boko Haram.

Tangu waasi wa Boko Haram kuanzisha uasi,kiasi ya watu 135,000 wametoroka kutoka eneo la kaskazini mashariki mwa Nigeria na kiasi ya wengine 850,000 wameachwa bila makaazi katika eneo hilo.

Read more...

Maaskofu Nigeria wasikitikia mauaji ya Boko Haram

BARAZA la Maaskofu Katoliki Nigeria limeeleza kuwa mauaji yanayofanywa na kundi la Waislamu wenye msimamo mkali nchini humo la Boko Haram ni ukatili dhidi ya binadamu.

Rais wa Baraza hilo, Askofu Mkuu Ignatius Ayau Kaigama alibainisha hayo katika taarifa iliyopatikana kutoka Vatican akielezea hali ilivyo katika nchi hiyo.

Askofu Mkuu Kaigama alisema mashambulizi hayo yanaendelea kuongezeka licha ya juhudi za Serikali ya Nigeria kupambana kwa dhati na vitendo vya kigaidi nchini humo. 

Alisema Boko Haram wanafanya mashambulizi ya kushtukiza kiasi kwamba inakuwa vigumu kwa vikosi vya ulinzi na usalama kudhibiti vitendo hivvyo vinavyoendelea kusababisha majanga kwa wananchi wengi wa Nigeria.

Askofu Mkuu Kaigama alisema Serikali haina budi kutekeleza wajibu wake wa kuhakikisha amani na utulivu vinarejea tena nchini Nigeria kwa kuzingatia utawala wa sheria.

Alisema hivi karibuni, Boko Haram waliua watu 35 waliokuwa kwenye msafara wa harusi na kueleza kuwa kundi hilo ni tishio kwa usalama, amani, utulivu na maendeleo ya wananchi wa Nigeria kwa sasa na kwa siku za usoni.

Rais huyo wa Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria alisema mwanzoni mashambulizi kama hayo yalikuwa yakielekezwa kwa Wakristo lakini sasa watu wengi wanaendelea kushambuliwa bila huruma.

Read more...
Tumaini Media

Radio-TV Tumaini, also trading as Tumaini Media, is legally registered in Tanzania under the Business Registration and Licensing Agency (Brela), No 116952. It is a registered Tax payer with TIN 100-251-094 and VRN 10-012753-P. Tumaini Media runs radio and TV stations, and a newspaper namely Radio Tumaini, Tumaini Television and Tumaini Letu, respectively. Tumaini Media seeks to serve the Tanzania community regardless of their colour. race. religion and tribe.

  Jesus is the Patron of our Station

We Now Covering 7 Regions

Coverage has been expanded to include seven out of 21 regions of Tanzania, thus: Tanga, Pwani, Morogoro, Zanzibar, Dar es Salaam and some areas of Dodoma, Kilimanjaro, Iringa and Mbeya Regions.