Menu
RSS

Kard. Pengo ataka waamini kuchangia ujenzi nyumba ya Askofu Bagamoyo

Kard. Pengo ataka waamini kuchangia ujenzi nyumba ya Askofu Bagamoyo

Na Editha Mayemba

ASKOFUMkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo amewaomba waamini wa jimbo hilo na wote wenye mapenzi mema kujitoa kuchangia ujenzi wa nyumba ya Askofu wa Jimbo jipya la Bagamoyo.

Alitoa ombi hilo katika salamu zake za shukrani kwa Mungu kwa kutimiza miaka 45 ya Upadri ambapo Mapadri wa Parokia mbalimbali za jimbo hilo wamempatia shilingi milioni 25 kwa ajili ya kumpongeza.

Kardinali Pengo alitoa kiasi hicho cha fedha alizozawadiwa Juni 20, mwaka huu pamoja na kiasi kama hicho kilichotolewa na watu mbalimbali na kufikia shilingi milioni 50 ili kuendeleza ujenzi wa nyumba hiyo.

Aliwashukuru wote waliochangia ujenzi wa nyumba hiyo na kuwaomba waamini wote bila kujali majimbo yao kutoa michango zaidi ili ujenzi huo ukamilike kwa wakati na kwamba yeyote atakayechangia fedha hiyo itatumika kama ilivyokusudiwa.

“Tunao Mradi wa ujenzi wa nyumba ya Askofu, Bagamoyo, ningekuwa kijana kiasi cha fedha nilichopewa na Maparoko ningeweza kununua pikipiki au baiskeli, lakini fedha zote ni nilizozipokea nitazipeleka kwenye ujenzi”

“Juni 19 Padri Valentino Bayo aliniita kwa shughuli ya uzinduzi wa Jiwe la Msingi la ujenzi huo. Tumeshatumia zaidi ya mililioni  500 katika awamu ya kwanza:

Jimbo Kuu la Dar es Salaam liliahidi kutoa sh. Mil 250 na nilikuwa bado sijapeleka hivyo nikijumuisha kiasi nilichokipokea nitawasilisha zote kwa pamoja na kila aliyechangia awe na hakina fedha zote zitatumika kama zilivyokusudiwa.”

Kardinali Pengo alimshukuru Mungu kwa zawadi kubwa ya miaka 45 ya Upadri kwani yeye ni miongoni mwa Mapadri saba walio baki hai kati ya Mapadri 25 waliopewa Daraja ya Upadri pamoja Juni 20, 1971.

“Kwamba nimetimiza miaka 45, siamini mimi mwenyewe naona ni kama tukio lilotokea juzi au jana, lakini nikichunguza wale tulioanza pamoja, tumebaki wachache sana:

Kati ya mapadri 27 tuliopata upadrisho mwaka ule (1971) kwa Tanzania nzima, tulio hai hatuzidi hata saba, wengine wametangulia mbele ya Mungu”, alisema na kuongeza:

“Hii inanipa nguvu kubwa ya kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa Baraka hiyo kubwa. Mwenyezi Mungu anapotoa baraka zake, anatoa na wajibu, najiuliza neema hii aliyonipa Mungu ya miaka 45 ya Upadri je niliyotenda yanalingana na uwingi wa miaka hiyo? Basi namuomba Mungu yale niliyopungukiwa anisamehe pamoja na wenzangu tulioanza pamoja mwaka ule”.

Alisema anaendelea kumuomba Mungu kiasi kilichobakia cha maisha yake hapa duniani aendelee kujitoa bila kujibakiza licha ya kuwa na umri wa zaidi ya miaka 70.

Kardinali Pengo alitumia nafasi hiyo kuwashukuru waamini wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam kwani katika miaka hiyo yote ametumikia kwa kiwango kikubwa Jimbo hilo tangu akiwa Padri Seminari ya Segerea na hata alipoteuliwa kuwa Askofu.

Aliwahimiza Mapadri kutokata tamaa kwa magumu wanayokutana nayo katika Utume wao na daima wamwombe Mungu neema ya kufurahia Upadri wao kwa kumwadhimisha Mungu daima.

Kardinali Pengo aliwashauri Mapadri kusali Sala ambayo yeye mwenyewe amekuwa akiitumia kwa kuwa sala hiyo itawasaidia kuomba neema ya kuendelea kufanya kazi hiyo katika hali yoyote.

“Katika miaka hiyo 45 hata siku moja sijawahi kujua kwa nini nilikuwa Padri, imekuwa ni chimbuko la furaja japo kuna magumu kadhaa unaweza kupanga kazi lakini haziendi kama ulivyopanga basi nachukulia ni mambo ya kibinadamu”.

“Napenda kuwaambia mapadri wenzangu kwamba, kamwe tusivunjike moyo, tusijutue kwamba kwa nini tuliamua kuwa mapadri, kila siku tuombe neema ya kufurahi upadri wetu hata katika mambo ya kufurahisha na yale magumu yanayoweza kutukatisha tamaa.

“Mimi daima ninayo sala kwa Kristo mwenyewe Kuhani Mkuu, Yesu ‘Ee Yesu mwema unifanyizie niwe Kuhani kulingana na Mapenzi ya moyo wako’ Sala hiyo Padri akiisali kadri iwezekanavyo kwa kila siku, nina hakika nguvu kutoka kwa Kristo zitamsimika kuweza kuendelea hata katika hali inapokuwa ngumu.

Kituo cha Tumaini Media kinamtakia Mwadhama Polycarp  Kardinali Pengo, heri na baraka za Mungu katika kumbukumbu yake ya Upadri, maisha marefu na afya njema alipoadhimisha mapema mwezi wa saba mwaka huu.

end 

back to top
Tumaini Media

Radio-TV Tumaini, also trading as Tumaini Media, is legally registered in Tanzania under the Business Registration and Licensing Agency (Brela), No 116952. It is a registered Tax payer with TIN 100-251-094 and VRN 10-012753-P. Tumaini Media runs radio and TV stations, and a newspaper namely Radio Tumaini, Tumaini Television and Tumaini Letu, respectively. Tumaini Media seeks to serve the Tanzania community regardless of their colour. race. religion and tribe.

  Jesus is the Patron of our Station

We Now Covering 7 Regions

Coverage has been expanded to include seven out of 21 regions of Tanzania, thus: Tanga, Pwani, Morogoro, Zanzibar, Dar es Salaam and some areas of Dodoma, Kilimanjaro, Iringa and Mbeya Regions.