Menu
RSS

Shirika la Wasalvatorian lapata viongozi wapya

MAPADRI MAPADRI

Na Lawrence Kessy, RCT

SHIRIKA la Mungu Mwokozi (Wasalvatoriani) Provinsi ya Tanzania, limefanya Mkutano wake Mkuu na kuwachagua viongozi wake wapya watakaoliongoza shirika hilo kwa kipindi cha maka mitatu ijayo.

Mkutano huo ulifanyika hivi  karibuni katika Prokura yao iliyopo Kurasini, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam na kufanikisha kupatikana kwa viongozi hao.

Mkutano huo ulitanguliwa na semina ya Kiroho iliyoongozwa na Abate Mstaafu wa Abasia ya Hanga, Abate Aqulini Nyirenda, O.S.B ambaye kwa sasa anafanya utume wake mjini Roma, Italia.

Katika Mkutano huo kwa kauli moja wanashirika walimchagua Padri Ponder Paulinus Ngilangwa, SDS kuwa Mkuu wa Shirika akichukua nafasi iliyoachwa wazi na Padri Africanus Lokilo, SDS aliyemaliza muda wake wa vipindi viwili mfululizo kuliongoza Shirika la Wasalvatoriani Tanzania.

Padri Ngilangwa, kabla ya uteuzi huo, alikuwa anasaidia malezi kwa waseminari, katika nyumba ya malezi ya Shirika Jimbo Katoliki la Morogoro, ambapo katika uongozi wake atashirikiana na washauri wengine wanne ambao ni Padri, Lazarus Vitalis Msimbe, SDS, kama Makamo Mkuu wa Shirika, Padri Eugene Reslinski, SDS, Padri Ayub Mwang’onda, SDS na Bruda Sylvester Chimoto, SDS, ambaye pia ni Mtunza hazina wa Shirika, waliochaguliwa katika mkutano huo.

“Nawashukuru wajumbe wa Mkutano huo kwa imani  na heshima kubwa mlionipa na kuniionesha kwangu, hadi kunipa majukumu makubwa na mazito ya kuliongoza Shirika, hasa kwa kipindi hiki ambacho Shirika letu linakabiliwa  na changamoto nyingi, kama vile za kitume, kimalezi, kielimu na kadhalika,” alisema Padri Ngilangwa.

Alisema aliwataka wanashirika hao kumpa ushirikiano, kwani akishindwa au akifaulu wote watakuwa wamechangia na bila ushirikiano hataweza kufanya miujiza kuleta maendeleo ya Shirika, na hasa suala zima la kuongeza maeneo mengine ya kitume katika Majimbo mbalimbali nchini Tanzania.

Kwa mujibu wa Padri Ngilangwa, SDS, ni wakati sasa kwa wanachama wote, wa Shirika la Mungu Mwokozi, kuchapa kazi kwa bidii na maarifa popote pale walipo, na kuacha kusema maneno bila utendaji wowote ule kwa manufaa ya Shirika zima na kutaka kila mmoja aone kuwa ana majukumu yake na mchango wake katika Shirika.

“Uzuri nawajua wote hapa na majina yenu yapo na ninayo na ninyi ndio mlionichagua na nitaanza na ninyi kuwapangia majukumu. Nitashangaa sana kama nitampa yeyote kati yenu hapa majukumu alafu akataee wakati ninyi wenyewe ndio mlionichagua”, alisema Padri Ngilangwa, SDS.

Padri Ngilangwa ni mzaliwa Juni 3, mwaka 1977 katika Jimbo Katoliki la Njombe na alijiunga na Shirika la Mungu Mwokozi mwaka 2000, akafunga nadhiri za kitawa 07/12/2002, nadhiri za daima 01/01/2009, na daraja Takatifu la Upadritarehe  04/06/2010.

Naye Mkuu wa Shirika hilo duniani kutoka Roma, Padri Milton Zonta, SDS aliwashukuru Wanashirika wote wa Provinsi ya Tanzania, kwa juhudi zao za utume hapa Tanzania na hata wale walioko nje ya Tanzania, kwa kazi nzuri wanazozifanya, kwani ndio lengo na karama ya Mwanzilishi wa Shirika hilo, Padri Francis Maria wa Msalaba Jordan.

 “Ninawashukuru viongozi wote waliomaliza muda wao kwa vipindi viwili, kwa kazi nzuri waliyoifanya kuendeleza majukumu mbalimbali ya Shirika kwa kipindi chote, ingawa mlikutana na magumu na changamoto nyingi, hamkukata tama katika hilo. Mungu awabarikini wote”, alisema Padri Zonta, SDS.

Pia aliwashukuru na kuwapongeza viongozi wote waliochaguliwa, kwa kukubali kwao kuyapokea majukumu makubwa ya Shirika na si kwa Kanisa la Tanzania tu bali, kwa Kanisa lote ulimwenguni, na kuahidi kushirikiana nao, katika kustawisha maendeleo ya Shirika kwa ujumla.

Padri Zonta, SDS aliwatakia Wanashirika wote utume mwema na maisha mema ya jumuiya yenye juhudi, maarifa, na mafanikio tele, kwani wanashirika wengi bado ni vijana ukilinganisha na sehemu nyingine za Shirika kama Ulaya na Amerika. Na kumwomba Roho Mtakatifu awe nao katika utume wao wa kila siku zote.

Shirika la Mungu Mwokozi (Wasalvatoriani) kawa hapa Tanzania, Makao Makuu ya Shirika yako Masasi katika Jimbo Katoliki la Tunduru -Masasi, na wanafanya utume wao katika Jimbo hilo la Tunduru -Masasi, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam na katika Jimbo Katoliki la Morogoro. 

back to top
Tumaini Media

Radio-TV Tumaini, also trading as Tumaini Media, is legally registered in Tanzania under the Business Registration and Licensing Agency (Brela), No 116952. It is a registered Tax payer with TIN 100-251-094 and VRN 10-012753-P. Tumaini Media runs radio and TV stations, and a newspaper namely Radio Tumaini, Tumaini Television and Tumaini Letu, respectively. Tumaini Media seeks to serve the Tanzania community regardless of their colour. race. religion and tribe.

  Jesus is the Patron of our Station

We Now Covering 7 Regions

Coverage has been expanded to include seven out of 21 regions of Tanzania, thus: Tanga, Pwani, Morogoro, Zanzibar, Dar es Salaam and some areas of Dodoma, Kilimanjaro, Iringa and Mbeya Regions.