Menu
RSS
Uchumi

Riba kwenye Taasisi za fedha

 

Na Dk. Felician Kilahama

Awali ya yote inanibidi kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa mema mengi anayotutendea katika maisha yetu. Vilevile, nikiri kwamba mimi sina utaalam wa masuala ya fedha au shughuli za kiuchumi.

Uelewa wangu ni mdogo kiasi kwamba yote nitakayoyasema hapa niombe radhi pale nitakapokuwa nimekosea. Inawezekana msomaji wa Makala hii akasema kuwa: iwapo huelewi au huna elimu ya kutosha juu ya masuala ya fedha na uchumi kwa nini usiulize ukaeleimishwa na wenye elimu hiyo? Mtazasamo wa namna hiyo ni sahihi hasa kwa yeyote anbaye nia yake ni kujifunza kwa faida yake binafsi.

Naelewa wako wengi wenye hali kama yangu na pengine wanahitaji kuelimishwa kwa namna moja au nyingine ili waweze kufanya maamuzi sahihi katika harakati za kujiletea maendeleo endelevu kama mtu binafsi, familia au hata kijamii.

Nimeonelea ni vizuri niyatoe mawazo yangu kupitia fursa hii ili atakayeguswa na jambo hili aweze kunielimisha na kwa kufanya hivyo inawezekana tukanufaika wengi kutokana na ukweli kwamba “elimu haina mwisho”.  Vilevile, nashukuru Uongozi wa gazeti hili kwa kukubali kuchapisha Makala hii kwa faida yetu sote.

Natambua kwamba binadamu hulazimika kuchukua hatua iwapo ataona kuna changamoto inayomkabili katika maisha ya kila siku. Mfano, kama kuna misitu au  miti ya kutosha siyo rahisi watu wengi, kwa utashi wao wenyewe, wakaamua kupanda miti. Iwapo itatokea watafanya hivyo msukumo wa ziada lazima utoke kwa wenye mamlaka juu yao na kwa kutumia nguvu ya sheria.

Kwa upande mwingine, iwapo hakuna miti na hali inakuwa ngumu kimaisha mfano kushindwa kupika chakula kwa sababu upatikanaji kuni au mkaa ni shida; haishangazi kuona wengi wanachukua hatua za kupanda miti ili hatimaye wapate chanzo cha nishati ya kupikia.  Hali ndivyo ilivyo kwa suala hili ninalolieleza hapa.

Kabala sijapata shida ya kujihusisha na vyombo vya fedha hususani benki; nilikuwa siwazii suala la kukopa au riba zikoje. Lakini baada ya changamoto ya mahitaji ya fedha kutugusa kifamilia ndipo hali ya kufikiri namna ya kujikwamua ikapelekea kuwaza kukopa katika taasisi za fedha hasa benki.

Hatua ya kwanza ilikuwa kupata maelezo kutoka benki ni jinsi gani mkopo unavyopatikana iwapo mtu anahitaji kukopa? Ni vigezo gani vinatumika kuweza kumpatia mteja mkopo anaouhitaji? Maelekezo ikawa ni lazima anayetaka kukopa awe na akaunti kwenye benki anayotaka kupata mkopo.

Vilevile, ni lazima afanye mchanganua wa kina namna mkopo utakavyotumika; kuonyesha jinsi utakavyorejeshwa na kuwepo ushahidi wa kuridhisha wa mali isiyohamishika kama shamba au nyumba na hatimiliki.

Shamba au nyumba  pamoja na hatimiliki ndiyo rasilimali ambazo benki itazitumia kama dhamana kwa mkopo. Kadhalika rasilimali hizo thamani yake (value of fixed assets) idhibitishwe kwa taarifa ya Mthamini mali anayeaminiwa na benki husika na atokane na kampuni au taasisi yenye makubaliano na benki kufanya kazi hiyo. Gharama ya kuthamini rasilimali hizo ni jukumu la mkopaji.

Kabla ya kupata mkopo sharti hili lazima litimizwe hata kama utapata mkopo au laa. Huu unakuwa mwanzo kwa mkopaji kupata maumivu ya  aina yake: huna fedha unataka ukope kakini masharti ya kukopa yanakupelekea kuanza kutumia fedha ambazo huna unazipata wapi?.

Ukiyatimiza hayo benki inakuwa iko tayari kujadiliana nawe na ikiridhika na mawasilisho mkopaji anapata fursa ya kukopeshwa kwa masharti ya kurejesha mkopo pamoja na riba kwa muda mtakaokubaliana. Baada ya kupata mkopo hapo ndipo maumivu zaidi yanapoingia kulingana na riba inayotozwa na jinsi ya kuurejesha mkopo.

Kwa waliowengi siyo rahisi kupata mkopo toka benki maana ni vigumu kukidhi masharti yanayotolewa kwa mkopaji. Vilevile, riba inayoambatana na mkopo ni kubwa sana kiasi cha kuwaumiza wakopaji kutokana na jinsi inavyokokotolewa katika mahesabu ya kila siku.

Kwa uelewa wangu mdogo nilitegemea kama nimekopa shilingi milioni 12 kwa kiwango cha riba ya asilimia 20 kwa mwaka na kulipa mkopo kwa muda wa miaka mitatu (miezi 36) ningetegea benki kufanya biashara kifaida lakini pia na mimi mkopaji kuwa na unafuu kidogo.

Kwa mfano nikirejesha kila mwaka shilingi milioni nne (4) pamoja riba isiyozidi shilingi milioni moja (jumla milioni tano) kwa miaka mitatu ningelipa milioni 15. Kwa hali hiyo benki inapata faida na mkopaji ananufaika kwa kutatua changamoto iliyokuwepo au pia kujiongezea kipato kupitia uwekezaji.

Kiuhaliasia mambo ni tofauti sana na matarajio ya mkopaji na ndipo maumivu yanapowakumba wakopaji. Hata kama haujakopa hali hii itakugusa kwa namna moja au nyingine kwa kusababisha gharama za maisha kupanda mara kwa mara (i.e. tunaponunua huduma mbalimbali na bidhaa kwenye soko unasikia bei zimepanda).

Katika hali ya kibenki unapokopa shilingi milioni 12 kwa miaka mitatu unajikuta unalipa zaidi ya shilingi milioni 17 (mkopaji anaizalishia benki shilingi milioni tano kwa miaka mitatu). Vilevile, kwa aliyekopa shilingi milioni 30 kutoka benki mojawapo hapa nchini na kwa kipindi cha miaka mitatu akajikuta analipa shilingi milioni 48 ikiwa ni marejesho ya mkopo na riba.

Cha kushangaza ni kwamba mkopaji analipa liwango hichohicho cha marehesho tangu mwamzao hadi mwisho. Nilitegemea kwa hali ya kawaida nikirejesha mkopo na riba baada ya mwaka nianze kulipa kiwango pungufu na baada ya miaka miwili nilipe kiwango pungufu

zaidi kwa sababu sehemukubwa ya mkopo na riba vimerejeshwa. Lakini kiwango cha marejesho kinabaki kilikile mwanzo hadi mwisho kulikoni?

Mfano mwingine ni aliyekopa shilingi milioni 100 na kutakiwa kurejesha mkopo huo ndani ya miaka miwili. Alianza kurejesha mkopo kwa kulipa shilingi zaidi ya milioni tano na laki saba kila mwezi. Atakapomaliza miaka miwili marejesho yaweyamemalizika na kwa hali hiyo atalipa benki si chini ya shilingi milioni 137.

 

Hii inamaana kwamba ndani ya kipindi hicho cha miaka miwili awe amelipa mkopo (shilingi milioni 100) na tozo ya riba (zaidi ya shilingi milioni 37). Hebu angalia kwa kipindi hicho kifupi mkopeshaji (bank) inapata shilingi milioni 37 kutokana na uwezo wake wa kumpatia mkopaji (mhitaji) shilingi milioni 100.

Iwapo mkopaji atayamudu mazingira magumu ya kibenki lazima awe na nafasi nzuri ya kutoa huduma au kufanya biashara ambayo itamwingizia faida ya kutosha. Mathalani mifano hiyo niliyoitoa biashara au huduma husika viweze kutoa tija ya kutosha kiasi kwamba kila shilingi aliyokopa na kuitumia imzalishie takribani senti hansini: yaani apate shilingi mia moja hamsini. Kinyume cha hapa atakuwa anafanya kazi isiyolipa hivyo hataweza kulipa mkopo na wakati huo atashindwa kujiendeleza.

Hali hiyo inamaanisha kwamba kwa muda wa miaka miwili mkopaji aweze kupata angalau shilingi milioni 150 ili alipe deni na riba na kuweza kupata faida pengine akapanua shughuli zake.  Katika haya yote mwisho wa siku anayeumia ni mlaji au mtumiaji wa huduma zinazotolewa na mhusika (mkopaji).

Hii ndiyo dhana kwamba aliye nacho ataongezewa na mwenye kidogo hata hicho kidogo atanyanganywa. Hivyo walionacho watazidi kutanua (mabenki kugawana mabilioni ya shilingi kama faida) wakati wakopaji wengine wakifilisiwa kwa kushindwa kurejesha mikopo waliochukua kwa kudhani wangejikwamua kutoka kwenye hali ya umaskini na kupiga hatua mbele.

Serikali ya awamu ya tano imedhamira kutuingiza kwenye uchumi wa viwanda. Hii ni nia njema maana kupitia shughuli za viwanda mkulina atanufaika kwa kuona mazao yake yananunuliwa na kusindikwa (hasa mazao yanayoharibika haraka kama matunda).

Wafugaji nao wataweza kupata soko la uhakika kwa bidhaa zitokanazo na mifugo. Pamoja na nia hiyo nzuri ya Serikali iliyopo madarakani ya kutaka kuinua uchumi wetu kwa nchi; mtu mmoja mmoja au familia na jamii; ipo changamoto kwamba baadhi ya wawekezaji wanapata mitaji yao kutoka benki na vyombo vingine vya fedha.

Iwapo hali ya riba ndiyo hiyo (gharama kubwa sana) wanapokopa na kuwekeza, bidhaa/huduma zitakazozalishwa zitauzwa kwa bei kubwa kuliko uwezo wa wanunuzi kwa maana wengi kipato kiko chini.

Hata kama mtu ameajiriwa bado viwango vya mishara viko chini kumwezesha kumudu gharama za maisha ya kila siku. Kwa hali hiyo ni dhahiri kwamba riba kwenye mikopo zikiendelea kuwa kubwa na wakati huo tunahitaji kupata huduma na bidhaa kwa bei nafuu; itabaki kuwa kitendawili kisichoteguliwa mwishowake ni kilio kwa watu wa kawaida wenye kipato cha chini.

 

Kimsingi mwenye madhara ni mnunuzi wa bidhaa au mtumiaji wa huduma takribani kwenye maeneo yote ya uchumi ambayo gharama zake zinalipwa kupitia mlaji au mtumiaji wa huduma husika.

Tumekuwa tunalia kwamba gharama za umeme zinatuumiza kwa sababu ziko juu; lakini wazalishaji wa umeme (TANESCO) na kuusambaza kwa watumiaji hujitetea kuwa gharama za kufanya kazi hiyo ni kubwa. Pengine nao wanakopa kuwekeza kwenye mitambo ya kufua umeme. Sasa riba kwa mikopo inapokuwa kubwa inakuwa vigumu kwa TANESCO kusambaza na kuuza huduma ya umeme kwa bei ya chini. Matokeo yake ni mtumiaji wa umeme kugharamia riba kwa mkopo kupitia bei kubwa tunazolipa kila mwezi.

Tunafahamu fedha zinazolipwa na TANESCO kwa kampuni kama IPTL na nyinginezo ni fedha nyingi sana sijui makubaliano yalivyokuwa lakini lazima walipe. Je, TANESCO fedha za kulipia madeni kama hayo inazipata wapi? Kwa vyovyote vile njia kuu ni kutoka kwa wateja wake ambao ni watumiaji wa umeme.

Wakati mwingine huwa ninafikiri kwamba Serikali itupunguzie makali ya gharama za umeme kwa kuipatia TANESCO ruzuku. Lakini ukija kwa upande mwingine ujiulize Serikali fedha za ruzuku inazipata wapi? Jibu ni kutoka kwa walipa kodi ambao ni watanzania wenye kufanya shughuli mbalimbali zinazowaingizia kipato wapate fedha za kulipa kodi.

Hata hivyo sote tunajikuta tumo katika mzunguko wa shida na changamoto kibao kutokana na mifumo ya benki pamoja na vyombo vingine vya fedha ilivyo. Hata ukiuangalia utaratibu wa kuuza na kununua fedha za kigeni hapa nchini umetoa uhuru sana wa watu kufanya wanavyotaka ili mradi wanufauke wenyewe bila kujali hali halisi ya walio wengi.

Haingii akilini mwananchi ndani ya taifa lake la Tanzania atakiwe kulipa malipo ya ada kwa kutumia fedha za Marekani (US Dollars) hasa katika shule zenye kutumia lugha ya kiingereza. Kwa nini hali iwe hivyo na shilingi yetu ikataliwe ni kwa maslahi ya nani?  Mifumo wa kifedha ilivyo inaweza ikawa kipingamizi mojawapo katika kufanikisha adhma ya kufikia uchumi wa kati ifikapo 2025.

Hali hii itaendela mpaka lini?  Ipo haja ya Serikali kupitia Benki Kuu na vyombo vingine vya fedha kuingilia kati suala la riba katika benki ya biashara ili kuwezesha watu wengi kukopa.

Kwa kweli tunahitaji kukopa ili tuweze kusonga mbele lakini iwapo wenye nacho watazidi “kuwakamua” wasionacho ambao ni wakopaji kupitia viwango vikubwa vya riba; maendeleo endelevu kwa jamii ya kawaida itakuwa shida kuyafikia ifikapo 2025 au 2030. Ni vigezo gani vinatumika kuweka riba kubwa kwenye mikopo wataalam wa masala ya fedha na uchumi wanalo jibu.

Pamoja na hayo jinsi mahesabu kuhusu mkopo na riba yake yanavyokokotolewa wakopaji, kwa kufahamu au kutokufahamu, tunajikuta mathalani mkopaji pengine unalipa zaidi ya asilimia 20 ya kile ulichokopa. Utaratibu wa Vikoba nao haujawa na nguvu za kutosha kumkomboa mtu wa hali ya chini.

Kwa kuwa kipato ni kidogo mkopaji kupitia Vikoba haruhusiwi kukopa zaidi ya mara tatu ya kiasi alichoweka kwenye Vikoba. Kwa maana hiyo bado tunahitaji huduma za kibenki

 

zitusaidie tusonge mbele kimaendeleo lakini kwa viwango vya riba vilivyo ni mtihani mgumu.

Maana mtu anaweza kupoteza maisha kutokana na “presha” ya damu (BP) kupanda iwapo benki itaanza kumdai kwa kushindwa kuurejesha mkopo pamoja riba yake. Mwenyezi Mungu atunusuru kwa hili kwa kuwapa hekima na busara viongozi wetu wakuu Serikali ili waweze kushughulikia suala hili kwa faida ya waliowengi.

Read more...

Utalii unavyoongeza mapato ya Taifa

·       Kituo kipya cha watalii chafunguliwa Kilwa

Dk. Felician Kilahama

Awali ya yote napenda kuchukua fursa hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya uhai na mema mengi anayonitendea hadi sasa.

 

 Kwa kweli Mwenyezi Mungu ni mwema sana kwetu na tunaendela kuishi tukipata riziki zetu au mkate wetu wa kila siku wakati mwingine kwa huruma yake Mungu kwetu maana hali kimaisha inazidi kuwa ngumu kila kukicha.

 

Hivyo ni jambo la kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kila wakati na kila mahali tutakapokuwa katika harakati za kujipatia riziki zetu za kila siku. Vilevile, namshukuru Mungu Mwenye enzi yote kwa kunijalia fursa na uwezo wa kutembelea Mkoa wa Lindi hususani Wilaya ya Kilwa.

 

 Nilikuwa wilayani Kilwa tangu tarehe 10 hadi 20 Januari 2016 na kufikia Mji Mdogo: Kilwa Masoko ambao ni Makao Makuu ya Wilaya ya Kilwa. Ingawa siyo mara yangu ya kwanza kufika Kilwa Masoko, lakini siku za nyuma sikuwahi kupata muda wa kutembelea maeneo kadhaa ndani ya Mji Mdogo Kilwa Masoko. Safari hii niliona ni vema kuweza kutenga muda kidogo na kuweza kuzuru sehemu mbalimbali katika eneo la Kilwa Masoko.

 

Kilwa ni moja ya Wilaya sita katika Mkoa wa Lindi na mpaka wake kwa upande wa Mashariki ni Bahari ya Hindi (Indian Ocean). Wilaya ilianzishwa wakati wa ukoloni mwaka 1942 wengi wetu tulikukwa hatujazaliwa na wakati ule taifa lilijulikana kama “Tanganyika” chini ya utawala wa Waingereza.

 

Kabla ya vita vya Dunia vya kwanza (First World War: 1914 hadi 1918) eneo la Africa Mashariki lilikuwa likitawaliwa na Wajerumani na lilijulikana kama “Dutch Oustefrica” likihusisha mataifa ya sasa Kenya na Uganda. Hata hivyo Tanganyika ilipata uhuru kutoka kwa Waingereza tarehe 9 Desemba 1961 na mwaka mmoja baadaye (tarehe 9 Desemba 1962) ikawa Jamhuri ya Tanganyika.

 

Tarehe 26 April 1964 mataifa ya Tanganyika na Zanzibar yaliungana na kuwa taifa moja la Tanzania (Jamhuri ya Muungano Tanzania) chini ya Serikali moja (United Republic of Tanzania-URT). Wilaya ya Kilwa ina ukubwa takribani hekta 1.4 millioni (1,390km2) za ardhi inayofaa kwa kilimo, ufugaji, pia kuna rasilimali nyingine kama maji, misitu, wanyamapori na kwa sensa ya watu ya 2012, Kilwa ina watu wapatao 171,000 wengi wao wakiishi vijijini.

 

Ilikuwa ni wiki ya pili ya mwezi January 2016 nikiwa Kilwa Masoko nikawa natembea hapa na pale ndipo nikaona jengo moja karibu na soko na stendi ya mabasi nikavutiwa na hivyo kuweza kufika hapo lilipojengwa.

 

Nilikuta wajenzi wanafanya kazi za kukamilisha ujenzi niliwauliza jengo ni mali ya nani na kwa shughuli gani? Jibu likawa ni mali ya Halmashauri ya Kilwa na litatumika kama kituo cha kuwapatia taarifa mbalimbali wageni na hasa Wataalii watakaotembelea Kilwa.

 

Kusema kweli baada ya maelezo hayo nikavutiwa na lengo hilo la kuweka kituo hicho hapo Kilwa Masoko maana vituo kama hivyo katika Wilaya za Mikoa ya Kusini mwa Tanzania ni nadra sana kuviona. Hii ina maana ni kituo cha aina yake kwa Mikoa ya Lindi na Mtwara pengine hata Mkoa wa Ruvuma. Baada ya hapo nilionana na Mratibu wa ujenzi wa Kituo hicho Bi Tatu Magina, ambaye alinifahamisha kuwa kituo kitazinduliwa rasimi tarehe 15 Januari, 2016 iwapo nitakuwa bado nipo Kilwa Masoko basi ninakaribishwa kushuhudia uzinduzi huo.

 

Hivyo niliona ni fursa nzuri kushiriki uzinduzi na kuweza kujifanza mengi kuhusu na masuala ya utalii katika Wilaya ya Kilwa na Wilaya jirani katika Mkoa wa Lindi na Mtwara mfano, Wilaya ya Newala inayopakana na Msumbiji pengine kupitia Mzumbiji tunaweza kupata Watalii na wageni wengineo wakaja wakatembelea Kilwa Masoko.

 

Ufunguzi rasimi wa Kituo cha Utalii Kilwa Masoko ulifanyika tarehe 15 Januari 2016 na Mgeni rasimi alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Kilwa Mheshimiwa Juma Njoway ambaye aliongozana na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Kilwa Bwana Hamidu Mtemekela.

 

Vilevile alikuwepo Mwenyekiti wa Mamlaka ya Mji Mdogo-Kilwa Masoko Bwana Ismail Slim na Mkuu wa Ofisi za Mambokale Kilwa Bwana Revocatus Bugumba. Wageni wengine mashuhuri waliohudhuria na pamoja na Bwana Olivier Coupleux, Mkuu wa Idara ya Uchumi na Urtawala katika Muungano wa Nchi za Ulaya (European Union Delegation to Tanzania).

 

Vilevile alikuwepo Bwana Philippe BonCour, Conseiller de cooperation et d’Action Culturelle ambaye aliwakilisha Ubalozi wa Ufaransa. Wizara ya Maliasili na Utalii iliwakilishwa na Bwana John Kimaro ambaye ni Mkurugenzi Msaidizi, Uhifadhi na Teknolojia, Idara ya Mambokale.

 

Wizara ya Fedha na Uchumi iliwakilishwa na Bwana Godlove Stephen ambaye ni Naibu Muidhinishaji (Deputy National Authorising Officer). Wakati huo Bodi ya Utalii Nchini (Tanzania Tourist Board- TTB) iliwakilishwa na Maafisa Waandamizi wawili kutoka Makao Makuu, Dar-Es-Salaam.

 

Mamlaka ya Kilwa Masoko pamoja na Halmashauri ya Wilaya kwa pamoja wameweza kujenga kituo hicho kwa msaada wa fedha na utalaam kutoka European Union Delegation in Tanzania pamoja na Ubalozi wa Ufaransa. Ujenzi wa kituo hicho uliafikiwa baada ya kuona kuwa Wilaya ya Kilwa inavyo vivutio vingi sana kwa ajili ya Watalii na wageni wengine.

 

Kwa mathalani, Kilwa kuna maeneo mazuri ya ufukweni mwa Bahari yanayofaa kwa watalii kuweza kupumzika, kuvinjari hapa na pale na hata kuogelea na kuvua samaki kiutalii siyo kibiashara. Vilevile, Kilwa kuna magofu ya Kale katika maeneo ya Songo Mnara, Kilwa Kisiwani na Kilwa Kivinje.

 

Maeneo hayo ni vivutio vizuri vya Utalii na tangu mwaka 1981 maeneo ya Kilwa Kisiwani na Songo Mnara yaliwekwa chini ya Urithi wa Dunia baada ya kuyatambua kuwa ni maeneo nyeti kihistoria na yanafaa kuhifadhiwa kitaifa na kimataifa kupitia Shirika na Umoja wa Mataifa (UN) la UNESCO.  

 

Kwa mwaka 2015 Halmashauri ya Kilwa kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mji Mdogo-Kilwa Masoko pamoja na Wizara ya Maliasili na Utalii pia kupitia uhisani wa Muungano wa Nchi za Ulaya (EU) waliweza kundaa Jarida: Karibu kilwa (Kilwa District Heritage Resources) lenye kurasa 75.

 

Jarida hilo limesheheni maelezo na picha zinazoonyesha rasilimali na urithi wa mambokale katika Wilaya ya Kilwa. Kupitia taarifa hiyo Watalii watakaotembela Kilwa Masoko na viunga vyake watapata mahali pa kuanzia kwa kupewa taarifa muhimu na kamili juu ya urithi asilia na vivutio vingine vinavyopatikana Kilwa.

 

Kilwa ni moja ya Wilaya za zamani sana katika nchi yetu na inapakana na Bahari ya Hindi (Indian Ocean) kwa upande wa Mashariki. Wageni kutoka Mashariki ya Kati na Mashariki ya Mbali hasa nchi za Uarabuni mfano, Oman, waliwahi kukaa Kilwa hata kabla ya Waingereza kuitawala Tanganyika (ambayo kwa sasa inajulikana kama Tanzania baada ya kuungana na Zanzibar na kuwa taifa moja.

 

Wakati huo Waarabu waliweza kufanya biashara ya kununua na kuuza Dhahabu na Meno ya Tembo (gold & ivory) trade). Ili kufanya shughuli za kibiashara vizuri waliweza kuanzisha na kutumia fedha ya Kilwa (Kilwa coins) ambayo ilirahisisha malipo husika. Baadaye ikaongezeka na biashara ya Watumwa na Kilwa Masoko ikawa sehemu maarufu Duniani.

 

Kilwa Masoko inaaminika kuwa ilianza kukaliwa na watu katika karne ya tisa (9). Kulingana na maelezao ya Bwana Olivier Coupleux, European Union waliweza kutoa msaada wa  500,000 Euros kwa ajili ya kujenga Kituo pamoja na kundaa Jarida lenye kuonyesha vivutia vinavyopatikana kwenye Wilaya ya Kilwa na mahali (locality) vinapopatikana).

 

 Aliongeza kuwa msaada huo kwa Wilayani Kilwa ni sehemu ya kiasi cha Euro millioni 10 zilizotengwa kwa ajili ya kusaidia Serikali kadhaa katika Bara la Africa ikiwemo Tanzania kuziongezea nguvu ya kuhifadhi na kuendeleza rasilimali kale na vivutio vya utalii. Kwa niaba ya Serikali yetu nawashukuru EU kwa msaada huo uliowezesha Mamlaka za Kilwa Masoko kujenga kituo cha kuhabarisha watalii na wageni.

 

Mwakilishi wa EU katika maelezo yake wakati wa kufunguliwa Kituo alisema kuwa Kilwa ina utajiri mkubwa wa rasilimali asilia na pia wa kihistoria. Hivyo akasema kuwa ifikapo mwaka 2025 namba ya Watalii watakoakuwa wanakuja kuitembelea Tanzania wakafika zaidi ya million nane.

 

Watalii wengi watapenda kufika Kilwa kwa sababu hata miundombinu itakuwa imeboreshwa sana. Kwa mfano, barabara pamoja na huduma za kiutalii kama hoteli na wakala wa kusafirisha na kuongoza watalii vitakuwa vimeboreshwa sana pamoja na kupatikana taarifa mbalimbali kwa Watalii. Kwa sasa inakadiriwa kuwa tunapata watalii karibu million moja kwa mwaka na wachache sana  wanaotembelea Kilwa.

 

Watu wengine muhimu ambao wamewahi kuitembelea Kilwa Masoko ni pamoja na Balozi wa Ufaransa Her Excellency Malika Berak, ambaye aliwahi kusema kuwa “the Kilwa heritage site holds extraordinary capital, both natural & cultural, for the local populations. It is on this capital that the sustainable development of the district must be built to make the ownership & today France takes part in project of sustainable development for Kilwa”.

 

Kwa Kiswahili alimaanisha kuwa Kilwa kuna urithi usio wa kawaida ikiwa ni pamoja na urithi wa kiasilia na kiutamaduni. Kwa urithi huo itakuwa rahisi kuwepo maeledeleo endelevu na sasa Ufaransa inashiriki katika harakati za kuleta maendeleo endelevi Wilayani Kilwa.

 

Kwa upande mwingine, Balozi wa Muungano wa Ulaya (the European Union Ambassador in Tanzania) His Excellency Filliberto Ceriani Sebregondi, kwenye Utangulizi wa Jarida la Karibu Kilwa (Kilwa District Heritage Resources) ambalo limeainisha maeneo mbalimbali yenye urithi asilia na utamaduni mahususi kwenye Wilaya ya Kilwa asisema: “cultural heritage preservation, creative industries, sustainable tourism management, and assistance for people to set up small & medium enterprises”.

 

Maneno haya ni ya kutia moyo kwa minsingi kwamba tukihifadhi utamaduni wetu, tukawa na ubunifu wa kiviwanda pamoja na kusimamia shughuli za utalii kwa misingi endelevu na kuwezesha jamii kuanzisha na kuendesha shughuli ndogo na za kati kijasilia mali tutaweza kuiona Wilaya ya Kilwa ikisonga mbele kijamii, kiuchumi na kimaendeleo kwa kutumia urithi wa tamaduni na rasilimalia asilia bila kuathithiri ubora wa mazingira.

 

Vilevile, Balozi Filliberto Ceriani Sebregondi aliongeza na kushauri kuwa: “the visitors who flock to Kilwa and enjoy the pristine beaches must prolong their stay for the people of Kilwa to fully benefit from their presence. Providing them with a diversified offering of natural & cultural attractions and increased tourist infrastructure will definitely contribute to this”.

 

Hapa Mheshimiwa Balozi ameshauri kuwa Watalii watakaopata fursa ya kutembelea Kilwa waweze kukaa muda wa kutosha; isiwe kufika leo na kesho kuondoka ili watu wa Kilwa waweze kunufaika na kuwepo Watalii wengi. Ili kufanikisha lengo hilo lazima tuhakikishe kuna vivutio vya kutosha vipo na vinafahamika kidunia.

 

Mfano, fukwe zenye mandhali nzuri kiasilia zitunzwe vizuri na kuwepo na miundombinu iliyoimara na bora ili Watalii waweze kupata huduma nzuri sawa na thamani ya fedha zao watakazolipa.

 

Kwa Kufanya hivyo wakazi wa Kilwa kwa kushirikiana na Serikali pamoja na sekta binafsi watafanikiwa na kupiga hatua mbele kimaendeleo kutokana na shughuli za Utalii endelevu.

 

Wakati wa ufunguzi wa Kituo cha kuendeleza Utalii Wilayani Kilwa Mgeni Rasimi  alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Kilwa Juma Njoway. Alitumia fursa hiyo kuwataka wananchi wa Kilwa watunze vizuri rasilimali za asili na utamaduni wao ili viweze kuwa vivutio tosha kwa Watalii na wageni watakaotembelea Kilwa kutoka sehemu mbalimbali duniani.

 

Vilevuile, aliwataka watakaosimamia Kituo hicho wahakikishe kinakuwa salama na kuendelezwa kila wakati ili kiendelee kuwa sehemu muhimu kwa Watalii na wageni wengineo kwa kuwapatia taafira muhimu watakazozihitaji.

 

Awali ya yote Mratibu wa shughuli za ujenzi wa Kituo Bi Tatu Magina, alitaarifu kuwa karibu asilimia 90 ya vifaa vilivyotumika kujenga Kituo vilitoka Wilayani Kilwa. Vilevile, Fundiwashi wote walitoka Kilwa na wamefanya kazi nzuri kama jengo linavyoonekana katika picha (sura ya nje na ndani ya jengo).

 

(Photos)

 

 Suala hili linaonyesha kuwa kwa namna moja au nyingine wakazi wa Kilwa wamenufaika na ujenzi wa Kituo. Kwa hiyo sehemu kubwa ya msaada uliotolewa na EU pamoja na Ufaransa (takribani Euro 500,000) zimetumika na kuwanufaisha wakati za Kilwa.

Akizungumza kwa niaba ya Wizara ya Maliasili na Utalii (MNRT), Bwana John Kimaro, Mkurugenzi Msaidizi katika Idara ya Mambokale, aliwashuru EU na Ubalozi wa Ufaransa kwa msaada wao wa fedha na utaalam hadi kuwezesha kupata jengo litakalotumika kwa shughuli za Mambokale na Urithi asilia na rasilimali Utamaduni katika Wilaya ya Kilwa.

 

Vilevile, alipongeza Uongozi wa Wilaya na Halmashauri pamoja na Mamlaka ya Mji Mdogo wa Kilwa Masoko kwa ushirikiano wao mzuri kwa kufanikisha mradi huo na aliongeza kuwa Wizara iko pamoja nao katika kuhakikisha kuwa Kituo hicho kinafanikisha malengo yake kwa kuzingatia utaratibu wa kisera, kisheria na kanuni.

 

Kituo sasa kimeanza na Waongoza Watalii sita (six Tour Guides) wanaume watano na mwanamke mmoja kiongozi wao akiwa Bwana Abdallah Ahmad. Wote wamepata mafunzo juu ya shughuli za kuongoza Watalii na wanafahamu lugha ya Kiingereza kiasi cha kuweza kumudu kazi zao za kila siku.

 

Hata hivyo litakuwa jambo jema kwa Kituo kuongeza Wataalam zaidi kadri namba ya Watalii itakavyoongezeka. Kituo pia kiweke utaratibu mzuri wa kuratibu shughuli za kiutalii kwa wananchi wanaokizunguka ili hatimaye waweze kunufaika na uwepo wa Kituo hicho Kilwa Masoko.

 

Pengine na Halmashauri ya Wilaya pamoja na Mamlaka ya Mji Mdogo Kilwa Masoko zitenge bajeti ambayo itasaidia kuendeleza shughuli za kituo hicho kila mwaka ikiwa ni pamoja na kukifanyia matengenezo ya mara kwa mara ili kuhakikisha kinakuwa imara na bora wakati wote.

 

End 

Read more...

Geita Gold Mine; Mgodi uliopania kuwakomboa wananchi kiuchumi

Na Charles  Msabila

Mgodi wa Dhahabu Geita GGM ulioko chini ya kampuni ya Anglogold Ashanti yenye makao yake makuu nchini AFRIKA ya Kusini,wenye migodi zaidi ya ishirini duniani kote na nimoja kati ya migodi mikubwa Afrika Mashariki na kati umeanza kutoa dhahabu rasmi mnamo mwaka 2000.

Michael van Anen Mkurugenzi mtendaji wa mgodi wa Geita GGM anasema kuwa moja kati ya kazi mhimu za mgodi wa Geita ni kuthamini na kuijali jamii inayotuzunguka ”Tunataka kuwekeza kwenye jamii na kuthamini sehemu tunapofanyia kazi”.  

Maeneo ambayo mgodi wa Geita unasaidia  ni yale yaliyoainishwa na Serikali ya Jamhuri ya Muugano wa Tanzania katika mpango wake wa Kukuza uchimi na kupunguza umaskini Tanzania (MKUKUTA) na moja kati ya maeneo hayo ni haya yafuatayo.

AFYA

Simon Shayo ambaye ni Makamu wa Rais AnglogoldAshannti (Geita Gold Mine -GGM)  anasema kuwa walishiriki kwenye ujenzi wa kituo cha Afya Bukole, Kasamwa, na wodi ya akina mama Hospitali ya mkoa Geita.

Mradi mwingine ulioanzishwa na Mgodi wa Geita ni Mountain Kilimanjaro Climbing Against Hiv And Aids Programme wenye lengo la kukusanya pesa za kuchangia na kupambana dhidi ya virusi vya UKIMWI  na UKIMWI. 

Simon Shayo katika kutoa taarifa kwa jamii alisema kuwa kila mwaka wana nia kwa ajili ya kukusanya pesa za kusaidia watoto, Akina Baba, akina mama, na jamii kwa ujumla walioguswa kwa namna moja ama nyingine na tatizo la virusi vya UKIMWI  na UKIMWI  na kuwafanya jamii waelewe kuwa  UKIMWI ni changamoto.

Shayo anasema kuwa Fedha inayotolewa na mradi huu kiasi fulani kinaenda Serikalini kupitia TACAIDS- Kamishna ya AIDS Tanzania na nyingine inakwenda kwenye taasisi mbalimbali Geita na kiasi kingine kinasaidia watoto yatima waliopoteza wazazi wao wote wawili kwa virus vya UKIMWI na mojawapo ya matumizi ya fedha hizi tayari kimeshajengwa kituo kikubwa cha watoto yatima cha Kaniosa Katoliki Jimbo katoliki la Geita kwa kushirikiana na halmashauri ya wilaya ya Geita.

Hadi sasa mfuko huu umeshasaidia zaidi ya mashirika 30. Pia mradi huu umejenga kituo cha ushauri Nasaha  cha Michungwani Tanga kwa kushirikiana na TACAIDS.  

Pia Mgodi wa Dhahabu wa Geita umesani mkataba wa miaka mtano kusaidia katika ujenzi wa mashua ya Kwanza ambayo ni Hospitali kwenye ziwa viktoria  kwa kushirikiana na Afrika Inland Church AICT na Vine Trust Jubilee hope Medical ambayo itakuwa inatoa pia matibabu ya Meno ambalo ni tatizo sugu kwa wakazi wanaozunguka ziwa viktoria.

Simon shayo  pia alisema kuwa wanajishughulisha  kuzuia na kutoa kinga ya mgonjwa mbalimbali katika jamii inayowazunguka kwa mfano, kugawa na kutoa vyandarua kwa wafanyakazi wote wa Mgodi na familia zao, kupulizia dawa ya kuua mbu kila nyumba ya mji wa Geita mradi ulioghjarimu zaidi ya shilingi milioni 1.3za Kitanzania tangu mwaka 2010 na umewanufaisha zaidi ya wakazi 20,000 kwenye mji wa Geita.

Shughuli nyingine ya kijamii ni kushirikiana na madaktari bingwa wa upasuaji kupitia mradi wa rafihki Surgical mission chini ya kampeni yake ya “ operation smile” kutoka nchi za Ulaya ambao wako katika hospitali ya mhimbili,CCBRT, Bugando na Seketule ambao wanafanya upasuaji maalum kwa wagonjwa wenye ulemavu maalum.

GGM wamekuwa wakigharimia gharanma zote ikiwemo usafiri,malazi, na chakula kuwapeleka wagonjwa hospitalini jijini Mwanza na kuwarudisha majumbani kwao.

ELIMU

Mgodi wa Dhahabu Geita umekuwa ukisaidia pia katika ujenzi waShule na Sekondari mkoani Geita.Moja ya shule hizo ni sekondari ya mfano ya Sayansi ya wasichana ya Nyenkumbu ambayo imegharimu zaidi ya shilingi za Kitanzania bilioni kumi nukta moja 10.1.

Shule hii ina malazi zaidi ya wanafunzi 900, Nyumba za kisasa za walimu na familia 36, wafanyakazi, Viwanja vya michezo, Maktaba, na Maabara za kisasa.

MAJI

Mgodi wa dhahabu Geita umechangia katika uchimbaji wa baadhi ya visima kwenye baadhi ya vijiji ili kupunguza ukali wa uhaba wa maji mkoani Geita kwa kushirikiana na Wizara ya maji ili kuhakikisha maji yanapatikana kwa ukaribu zaidi.

Tangu mwaka 2009 Mgodi wa dhahabu Geita kwa kushirikiana na Wizara yamaji mkoani geita walikubaliana kujenga mradi wa maji ambao ungegharimu Bilioni 8 za kitanzania kujenga mradi huu kutoka eneo la Bwawa la Nyaikanga mpaka Geita mjini. Na wamejenga tenki la maji lenye ujazo wa lita milioni tano 5.

ULIPAJI KODI

Mgodi wa Dhahabu Geita umechangia zaidi ya shilingi bilioni 957 za Kitanzania tangu mwaka 2000 mkoani Geita.

Kwa mwaka 2012 mpaka2013  GGM pekee ulichangia karibu bilioni 450 za Kitanzania serikalini za kodi.

Simon shayo anasema”   Zaidi ya shilingi bilioni 950 za Kitanzania zimelipwa katika kodi, na hii ni kwa mkoa wa Geita peke yake tangu mwaka 2000. Mgodi wa Dhahabu Geita umelenga kuhakikisha bidhaa zote zinazoweza kununuliwa Tanzania zinanunuliwa Tanzania isipokuwa pale tu ambapo haziopatikani Tanzania ili kujenga uchumi mbadala”.

Mnamo Agosti2013, Jitihada za mgodi wa geita za kuwekeza na kusaidia jamii zilipata heshima kwa kutunukiwa zawadi na Mheshimiwa Rais ,zawadi ijulikanayo kama Large Scale Mineral Projects Presidential Awards Csre 2012 Second Winner.

AJIRA

Mgodi wa Dhahabu Geita umetoa ajira kwa zaidi ya vijana 400 hasa kwa maeneo yanayozunguka mji wa Geita. Pia unagawa ajira 1600 za papo kwa papo na ajira 2000 kupitia kwa makontrakta  na wasambazaji.

Simoni anasema kuwa zaidi ya asilimia 95% ya waajiliwa katka mgodi wa Geita ni Watnzania na kwamba mgodi una lengo maalum kupunguza waajiliwa wa kigeni ili kutoa nafasi kwa wazawa. Mgodi una mpango mahsusi ili kuhakikisha kuwa asilimia 97% ya waajiliwa hadi kufikia mwaka 2016 ni watanzania.

Mfano mzuri ni Simon Shayo ambaye ni mtanzania aliyejiunga kwenye Kampuni akiwa ni msimamizi mwangalizi na sasa ni Makamu wa Rais Anglogold ashanti- Geita Gold Mine.

Hivyo matumaini yaliyopo ni kuona watanzania wanakuwa viongozi wakubwa katika kampuni ya Anglogold Ashanti.

Read more...

Magari yenye picha za rais yakamatwa

Licha ya rais wa Kenya Uhuru Kenyatta kuruhusu magari yanayobeba abiria nchini Kenya kuchorwa ama hata kupaka rangi yoyote ile,mabasi mawili yaliochorwa picha yake yamekamatwa na maafisa wa polisi mjini Mombasa Kenya.

Maafisa wa trafiki mjini Mombasa waliyakagua magari hayo na kuyakamata magari yote yaliokuwa yamechorwa picha pamoja na magari yenye madirisha yasioonyesha ndani.

Magari sita yakiwemo mawili yaliokuwa na picha ya Uhuru yalikamatwa,licha ya agizo la rais kuruhusu wamiliki wa matatu kuchora picha katika magari.

Uhuru alikuwa amesema kuwa hatua hiyo itawasaidia vijana kutumia vipaji vyao ili kuweza kujinufaisha kimaisha.

Uchoraji katika magari hayo na muziki ulipigwa marufuku mnamo mwaka 2003 na aliyekuwa waziri wa uchukuzi John Michuki.

Read more...

Mambo haya hatari katika elimu nchini

KATIKA kipindi cha hivi karibuni vichwa vya watanznia viliweza kukorogwa baada ya kuwepo kwa mkanganyiko wa kauli kuhusu mfumo mpya wa usahihishaji ama wa upangaji wa madaraja kwa wanafunzi wa Sekondari.

Hali hiyo imewatia wasiwasi mkubwa wadau wa elimu na kuielezea kama sehemu ya kuvuruga na kudidimiza kiwango cha elimu nchini kwa sababu wizara nyeti kama hiyo imekuwa ikiyumba katika utoaji wa kauli zake.

Itakumbukwa kwamba Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Sifuni Mchome alitangaza alama zinaonesha kwamba

 

A=75-100,B+=60-74,B=50-59,C=40-49,D=30-39,E=20-29, na F=0-19,

huku alama endelevu upimaji wanafunzi shuleni yani Continuous Assessment (AC) ikiwa ni 40 huku mtihani wa mwisho ukichangia alama 60.

Na kabla ya Serikali kutangaza alama hizo mpya wizara yenye dhamana na masuala ya Elimu nchini, iliunda Kamati iliyopewa jukumu maalum la kufanya uchunguzi na kuja na mapendekezo ya viwango vipya vya ufaulu na utaratibu wa CA.

Kwa hakika kamati hiyo ilifanya kazi hiyo na kuwasilisha ripoti yake wizarani Septemba mwaka huu ikiainisha kama ifuatavyo: A=80-100,B=70-79,C=50-59,D=40-49,E=35-39 na F=0-34 huku wakitaka CA iwe alama 25.

Hali hii inatajwa na wanazuoni kwamba kwa alama hizo za ufauli Tanzania inaweza kuwa nchi ya kwanza duniani kwa kuwa na alama za chini zaidi za ufaulu.

Aidha jambo lingine ambalo limewachanganya zaidi wananchi na wadau wa elimu ni ile ya kufuta daraja sifuri na kuongeza daraja la tano ama Five.

Lakini Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philip Mulugo, bungeni mjini Dodoma, naye alitoa kauli yake akisema kwamba daraja sifuri halijafutwa. 

Ni jambo la kushanga umma hasa katika mustakabali mzima wa ukuzaji na uboreshaji wa kiwango cha elimu nchini kuona kwambna kumekuwan na kauli za kupishana kuhusu jambo hilo.

Ni vizuri masuala hayo ya kitaalam yasiingizwe siasa kwani, ni dhahiri kwamba taifa litapata wataalam ambao hawataleta tija nchini na hatakuwa na ushindani na wenzao na hivyo taifa kuendelea kuwa nyuma.

Hakika hali hii pia itafanya Tanzania isiweze kuwa na watu wenye kugundua vitu na badala yake itakuwa ni watu wanaosoma kwa lengo la kupata ajira na kupokesha mshahara ili maisha yaende.

Kimsingi elimu ndiyo inayofanya taifa lolote lile liwe na maendeleo kwa sababu ya kuwepo kwa wataalama waliobobea, taifa kama Singapore, limeweza kupiga hatua kubwa katika masuala ya maendeleo na teknolojia na kuwa miongoni mwa mataifa yenye kuzalisha bidhaa mbalimbali ni kwa sababu ya kusimama vema katika elimu.

Hivyo Serikali isifanya mzaa na suala la elimu. Itakumbukwa kwamba mwaka huu wanafunzi wa Darasa la saba wamefanya mitihani yao na matokeo yametoka, lakini bado wadau wa elimu wanaendelea kusema kwamba mfumo wa elimu nchini bado hauna matunda ya moja kwa moja katika utoaji wa elimu bora kwa wananchi.

Aidha wadau hao pamoja na mambo mengine wamesema Serikali inatakiwa kuhakikisha inaboresha mfumo wa elimu ili kuwafanya watoto wa maskini waweze kupata elimu bora inayolingana na wanayopata watoto wa vigogo na watu wenye uwezo wanaosomeshwa nje ya nchi.

Kutokana na kutowepo kwa mfumo madhubuti katika sekta ya elimu, taifa linashindwa kupata wataalam wazuri katika kada mbalimbali na badala yake inategemea watu waliosoma nje ndio waje kuwa viongozi ama wataalama kutokana na elimu nzuri waliyoipata nje.

Hali ya watoto wa wakubwa na wenye kipato kikubwa kusoma nje kunadhihirisha wazi kwamba elimu ya Tanzania sio bora na hivyo kutaka watoto wao wasome nje ya nchi ili wapate elimu bora na badaye kuwa viongozi wa nchi.

Kama Tanzania itasimama vema na kutoa elimu bora tutatengeneza hata watu wa nje kuleta watoto wao waje kusoma Tanzania kwa sababu elimu itakuwa bora.

Lakini kama kila mmoja anatamani mtoto wake akasome nje ama shule maalum za International hakika taifa hili litafika pabaya sana, serikali ijipange ifanye maboresho na usimamizi wa karibu katika kutekeleza yale yaliyoamuriwa mambo yatakuwa mazuri.

Nchi kama za Kenya na Uganda ambako Watanzania wengi wanawapeleka watoto wao wakasome huko wamefanya mambo mazuri ya kuwa na mfumo bora ya elimu ikiwemo malipo na posho nzuri kwa walimu jambo linalofanya elimu kuimarika.

 

MPANGO WA BIG RESULT NOW 

Kuhusu Mpango wa Serikali wa kuongeza ufaulu kwa wanafunzi katika mpango wake wa Big Result Now, mpango huo unaweza kuwa wa kisiasa endapo mfumo wenyewe wa elimu hautaboreshwa vema.

Ni vema walimu wakaboreshewa maslahi yao na kutengeneza mifumo mizuri ya elimu hasa suala la miundombinu ili mpango huo uweze kutekelezwa vema.

Sio rahisi kuutekeleza vema mpango huo kama shule zingine wanafunzi wakiendelea kukaa chini huku zikiwa na mwalimu mmoja ama wawili jambo linaloweza kukwamisha mpango huo.

 

SHULE ZA KATA

Haya shule nyingi za Sekondari za Kata zilizoanzishwa katika mpango wa kila Kata kuwa na Sekondari yake, nyingi hali yake katika miundombinu na hata walimu bado hazijasimama vema hivyo zinaweza sisifanye vizuri katika utekelezaji wa mpango wa Big Result Now.

Tuhakikishe walimu wamelipwa madai yao, na wana malupulupu ya kutosha yaliyo bora yatakayowafanya wafanye kazi kwa moyo wa dhati, kwani wapo walimu kutoka Kenya na Uganda wanaofundisha Sekondari hapa nchini wakilipwa vema na kupewa kila kitu na ndiyo maana shule za binafsi zinafanya vizuri. 

Kama haya yatakuwa sawa kabisa hakika kuingiza mpango huo itakuwa wakati muafaka, lakini kama bado shida ipo hii ni sawa na bure.

RUSHWA KATIKA ELIMU

Suala la rushwa isipoangaliwa linaweza likachangia kutopatikana kwa matokeo makubwa kutokana na kuwepo kwa watendaji wasio waaminifu wanaodiriki kuuza mitihani ya taifa ili kujipatia chochote.

Katika ripoti yake Shirika la Transparency International linaonesha kuwa vitendo vya rushwa vimekithiri kwa kiasi kikubwa nchini Tanzania.

Ripoti hiyo pia pamoja na mambo mengine imeonesha kuwepo kwa vitendo vya ufisadi ambavyo vimeshamiri zaidi katika nchi ya Tanzania na Uganda ambapo takribani asilimia 70 ya watu wanaamini kushamiri kwa ufisadi.

Kwa mujibu wa Transparency International, sekta ya elimu ni miongoni mwa maendeo yenye kukabiliwa na vitendo vya rushwa kwa kiwango kikubwa.

Hivyo suala la watu kufaulishwa katika mitihani yao, kwa mtindo wa kutoa rushwa, iwe ya ngono ama fedha ni mambo mabaya yanayoweza kurudisha nyuma juhudi za serikali katika kuboresha elimu.

Na hata wataalama watakaopatikana hawatakuwa watu wa ukweli ambao taifa linaweza kuwategemea, na hali hii inaweza kuchangia majanga mengi kama vile ujenzi wa majengo yasiyo na viwango na barabara ambazo hubomoka baada ya muda mfupi.

Hii ni hali ya hatari ambayo Serikali inatakiwa kuiangalia kwa undani na kuchukua hatua madhubuti katika kunusuri elimu nchini.

Read more...
Tumaini Media

Radio-TV Tumaini, also trading as Tumaini Media, is legally registered in Tanzania under the Business Registration and Licensing Agency (Brela), No 116952. It is a registered Tax payer with TIN 100-251-094 and VRN 10-012753-P. Tumaini Media runs radio and TV stations, and a newspaper namely Radio Tumaini, Tumaini Television and Tumaini Letu, respectively. Tumaini Media seeks to serve the Tanzania community regardless of their colour. race. religion and tribe.

  Jesus is the Patron of our Station

We Now Covering 7 Regions

Coverage has been expanded to include seven out of 21 regions of Tanzania, thus: Tanga, Pwani, Morogoro, Zanzibar, Dar es Salaam and some areas of Dodoma, Kilimanjaro, Iringa and Mbeya Regions.